Jumapili, 26 Juni 2016

Rais John Magufuli afanya mabadiliko ya Wakuu wa Mikoa na kuwateua Wakuu wa Wilaya 139


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Juni, 2016 amefanya mabadiliko madogo katika safu ya wakuu wa mikoa na amewateua wakuu wa wilaya 139.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema katika mabadiliko hayo Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Bi. Zainab R. Telack kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Bi. Zainab R. Telack anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Anna Kilango Malecela ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Rais Magufuli pia amemteua Dkt. Binilith Satano Mahenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Dkt. Binilith Satano Mahenge anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Said Thabit Mwambungu ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es salaam ambako atapangiwa majukumu mengine.

Aidha, Rais Magufuli amemteua Dkt. Charles F. Mlingwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Dkt. Charles F. Mlingwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Stanslaus Magesa Mulongo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Wakuu wapya wa mikoa walioteuliwa wataapishwa tarehe 29 Juni, 2016 saa tatu kamili asubuhi Ikulu Jijini Dar es salaam na mara baada ya kuapishwa watakula kiapo cha maadili ya uongozi.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Juni, 2016 amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 139.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema katika uteuzi huo Rais Magufuli amezingatia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na umri ambapo kwa wale ambao umri wao ni zaidi ya miaka 60 ameamua wastaafu.

Mhe. Rais amewashukuru sana kwa utumishi wao mzuri na amesema pale ambapo itahitajika, serikali itaendelea kuwatumia katika majukumu mengine.

Katika uteuzi huo, Wakuu wa Wilaya waliopo sasa ambao wamebaki katika nafasi zao ni 39. Pia Rais Magufuli amewateua Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri 22 kuwa Wakuu wa Wilaya kutokana na utendaji wao mzuri.

Aidha, nafasi 78 za uteuzi wa Wakuu wa wilaya zimejazwa na watanzania wengine ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza wengi wao wakiwa ni vijana, wenye elimu ya kutosha na uzoefu katika maeneo mbalimbali.

Walioteuliwa kuwa wakuu wa wilaya ni kama ifuatavyo (Orodha imepangwa kulingana na mikoa)

ARUSHA
Arusha - Mrisho Mashaka Gambo
Arumeru - Alexander Pastory Mnyeti
Ngorongoro - Rashid Mfaume Taka
Longido - Daniel Geofrey Chongolo
Monduli - Idd Hassan Kimanta
Karatu - Therezia Jonathan Mahongo

DAR ES SALAAM
Kinondoni - Ally Hapi
Ilala - Sophia Mjema
Temeke - Felix Jackson Lyaviva
Kigamboni - Hashim Shaibu Mgandilwa
Ubungo - Hamphrey Polepole

DODOMA
Chamwino - Vumilia Justine Nyamoga
Dodoma - Christina Solomon Mndeme
Chemba - Simon Ezekiel Odunga
Kondoa - Sezeria Veneranda Makutta
Bahi - Elizabeth Simon
Mpwapwa - Jabir Mussa Shekimweli
Kongwa - John Ernest Palingo

GEITA
Bukombe - Josephat Maganga
Mbogwe - Matha John Mkupasi
Nyang'wale - Hamim Buzohera Gwiyama
Geita - Herman C. Kipufi
Chato - Shaaban Athuman Ntarambe

IRINGA
Mufindi - Jamhuri David William
Kilolo - Asia Juma Abdallah
Iringa - Richard Kasesela

KAGERA
Biharamulo - Saada Abraham Mallunde
Karagwe - Geofrey Muheluka Ayoub
Muleba - Richard Henry Ruyango
Kyerwa - Col. Shaban Ilangu Lissu
Bukoba - Deodatus Lucas Kinawilo
Ngara - Lt. Col. Michael M. Mtenjele
Missenyi - Lt. Col Denis F. Mwila

KATAVI
Mlele - Rachiel Stephano Kasanda
Mpanda - Lilian Charles Matinga
Tanganyika - Saleh Mbwana Mhando

KIGOMA
Kigoma - Samsoni Renard Anga
Kasulu - Col. Martin Elia Mkisi
Kakonko - Col. Hosea Malonda Ndagala
Uvinza - Mwanamvua Hoza Mlindoko
Buhigwe - Col. Elisha Marco Gagisti
Kibondo - Luis Peter Bura

KILIMANJARO
Siha - Onesmo Buswelu
Moshi - Kippi Warioba
Mwanga - Aaron Yeseya Mmbago
Rombo - Fatma Hassan Toufiq
Hai - Gelasius Byakanwa
Same - Rosemary Senyamule Sitaki

LINDI
Nachingwea - Rukia Akhibu Muwango
Ruangwa - Joseph Joseph Mkirikiti
Liwale - Sarah Vicent Chiwamba
Lindi - Shaibu Issa Ndemanga
Kilwa - Christopher Emil Ngubiagai

MANYARA
Babati - Raymond H. Mushi
Mbulu - Chelestion Simba M. Mofungu
Hanang' - Sara Msafiri Ally
Kiteto - Tumaini Benson Magessa
Simanjiro - Zephania Adriano Chaula

MARA
Rorya - Simon K. Chacha
Serengeti - Emile Yotham Ntakamulenga
Bunda - Lydia Simeon Bupilipili
Butiama - Anarose Nyamubi
Tarime - Glodious Benard Luoga
Musoma - Dkt. Vicent Anney Naano

MBEYA
Chunya - Rehema Manase Madusa
Kyela - Claudia Undalusyege Kitta
Mbeya - William Ntinika Paul
Rungwe - Chalya Julius Nyangidu
Mbarali - Reuben Ndiza Mfune

MOROGORO
Gairo - Siriel Shaid Mchembe
Kilombero - James Mugendi Ihunyo
Mvomero - Mohamed Mussa Utali
Morogoro - Regina Reginald Chonjo
Ulanga - Kassema Jacob Joseph
Kilosa - Adam Idd Mgoyi
Malinyi - Majula Mateko Kasika

MTWARA
Newala - Aziza Ally Mangosongo
Nanyumbu - Joakim Wangabo
Mtwara - Dkt. Khatibu Malimi Kazungu
Masasi - Seleman Mzee Seleman
Tandahimba - Sebastian M. Walyuba

MWANZA
Ilemela - Dkt. Leonald Moses Massale
Kwimba - Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon
Sengerema - Emmanuel Enock Kipole
Nyamagana - Mary Tesha Onesmo
Magu - Hadija Rashid NyemboUkerewe - Estomihn Fransis Chang'ah
Misungwi - Juma Sweda

NJOMBE
Njombe - Ruth Blasio Msafiri
Ludewa - Andrea Axwesso Tsere
Wanging'ombe - Ally Mohamed Kassige
Makete - Veronica Kessy

PWANI
Bagamoyo - Alhaji Majid Hemed Mwanga
Mkuranga - Filberto H. Sanga
Rufiji - Juma Abdallah Njwayo
Mafia - Shaibu Ahamed Nunduma
Kibaha - Asumpter Nsunju Mshama
Kisarawe - Happyness Seneda William
Kibiti - Gulamu Hussein Shaban Kifu

RUKWA
Sumbawanga - Dkt. Khalfan Boniface Haule
Nkasi - Said Mohamed Mtanda
Kalambo - Julieth Nkembanyi Binyura

RUVUMA
Namtumbo - Luckness Adrian Amlima
Mbinga - Cosmas Nyano Nshenye
Nyasa - Isabera Octava Chilumba
Tunduru - Juma Homela
Songea - Polet Kamando Mgema

SHINYANGA
Kishapu - Nyambonga Daudi Taraba
Kahama - Fadhili Nkulu
Shinyanga - Josephine Rabby Matiro

SIMIYU
Busega - Tano Seif Mwera
Maswa - Sefu Abdallah Shekalaghe
Bariadi - Festo Sheimu Kiswaga
Meatu - Joseph Elieza Chilongani
Itilima - Benson Salehe Kilangi

SINGIDA
Mkalama - Jackson Jonas Masako
Manyoni - Mwembe Idephonce Geofrey
Singida - Elias Choro John Tarimo
Ikungi - Fikiri Avias Said
Iramba - Emmanuel Jumanne Luhahula

SONGWE
Songwe - Samwel JeremiahIleje - Joseph Modest Mkude
Mbozi - Ally Masoud Maswanya
Momba - Juma Said Irando

TABORA
Nzega - Geofrey William Ngudula
Kaliua - Busalama Abel Yeji
Igunga - Mwaipopo John Gabriel
Sikonge - Peres Boniphace Magiri
Tabora - Queen Mwashinga Mlozi
Urambo - Angelina John Kwingwa
Uyui - Gabriel Simon Mnyele

TANGA
Tanga - Thobias Mwilapwa
Muheza - Mhandisi Mwanaisha Rajab Tumbo
Mkinga - Yona Lucas Maki
Pangani - Zainab Abdallah Issa
Handeni - Godwin Crydon Gondwe
Korogwe - Robert Gabriel
Kilindi - Sauda Salum Mtondoo
Lushoto - Januari Sigareti Lugangika

Wakuu wote wa Wilaya walioteuliwa wanapaswa kufika Ikulu Dar es salaam siku ya Jumatano tarehe 29 Juni, 2016 saa tatu kamili asubuhi kwa ajili ya kiapo cha maadili ya uongozi na maelekezo mengine kabla ya kuapishwa na wakuu wa mikoa watakaporejea katika mikoa yao.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Juni, 2016

Jumapili, 5 Juni 2016

Bondia MUHAMMAD ALI na Diplomasia ya TANZANIA

Tanzania imekuwa ikifuata sera ya kutofungamana na upande wowote tangu miaka ya 1960 mpaka sasa. Hali hiyo imeifanya Tanzania kuwa na uhusiano na pande zote mbili wakati wa Vita Baridi (Cold War).

Vita Baridi ni mvutano wa kisiasa na kijeshi baina ya Kambi ya Magharibi (Western Bloc) iliyoongozwa na Marekani na Kambi ya Mashariki (Eastern Bloc) iliyoongozwa na Urusi (USSR). Marekani na wenzake walifuata uchumi wa kibepari (capitalist economy) wakati Urusi na washirika wake wakifuata uchumi wa kijamaa (socialist economy). Mvutano huo ulianza mara baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia (WW II) hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Mwaka 1979 Urusi (USSR) iliivamia Afghanistan. Marekani ilipinga vikali kitendo hicho. Wakati huohuo Urusi ilikuwa inafanya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ambayo ilipangwa kufanyika jijini Moscow mwaka unaofuata 1980.

Ili kupata uungwaji mkono kukwamisha michezo hiyo ya olimpiki jijini Moscow mwaka 1980, Marekani ilianza kampeni zake kushawishi baadhi ya nchi zisishiriki mashindano hayo. Katika kujaribu kufanikisha hilo, rais wa Marekani wa wakati huo Jimmy Carter alimtuma bondia MUHAMMAD ALI kutembelea baadhi ya nchi ili aweze kuzishawishi zisusie mashindano hayo maarufu duniani.

Mnamo tarehe 2 Februari 1980 MUHAMMAD ALI aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (DIA) nchini Tanzania na kulakiwa na Chediel Mgonja, Waziri wa Utamaduni, Vijana na Michezo. MUHAMMAD ALI alipaswa kulakiwa angalau na Waziri wa Mambo ya Nje kwa kuwa ujio wake nchini Tanzania ulikuwa wa kidiplomasia na siyo michezo.

Lengo kuu la bondia huyo lilikuwa kuwasilisha ujumbe wa Rais wa Marekani Jimmy Carter kwa Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanzania wakati huo. ALI alitaka amshawishi Mwalimu Julius Nyerere ili Tanzania isishiriki Michezo ya Olimpiki iliyopangwa kufanyika jijini Moscow, Urusi mwaka huo. Pamoja na jitihada nyingi zilizofanywa na maafisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kumshawishi Mwalimu Julius Nyerere kuonana na mwanamasumbwi MUHAMMAD ALI, Mwalimu Nyerere alikataa kabisa ombi hilo.

Baada ya 'bondia mwanadiplomasia' MUHAMMAD ALI kushindwa kuonana na Mwalimu Julius Nyerere, aliamua kuondoka nchini Tanzania na kuelekea nchini Kenya ambapo alilakiwa na Rais Daniel Arap Moi. Kenya ilikubali ushawishi wa Marekani na kususia Michezo ya Olimpiki ya mwaka huo. Tanzania ilikataa ushawishi wa Marekani na kushiriki Michezo ya Olimpiki jijini Moscow, Urusi mwaka huo ambapo ilijinyakulia medali mbili za fedha kupitia wanariadha mashuhuri Suleiman Nyambui na Filbert Bayi.

Diplomasia huhitaji ushawishi. Marekani ilimtumia bondia MUHAMMAD ALI kutokana na umaarufu wake kipindi hicho na pengine kwa kuwa ni Mmarekani mweusi ili nchi za Afrika zishawishike kirahisi. Pia itakumbukwa mwaka 1974 Rais wa Zaire (sasa DRC) Mobutu Seseseko aliandaa mpambano mkali baina ya mabondia wa Marekani MUHAMMAD ALI na George Foreman. Mpambano huo maarufu uliotajwa kuwa "mpambano mkubwa wa karne ya 20" uliofanyika Kinshasa, Zaire na kupewa jina la 'THE RUMBLE IN THE JUNGLE.' ALI alishinda katika mpambano huo kumwongezea umaarufu mkubwa barani Afrika na duniani kote.

Tanzania haikuwa na maslahi yoyote katika uvamizi wa Urusi nchini Afghanistan. Pia Tanzania haikuona sababu yoyote kwanini ikubali ushawishi wa Marekani kususia Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1980. Haya yote yametokana na sera kigeni ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote. Tanzania imekuwa ikifuata sera hiyo tangu miaka ya 1960. Sera hiyo imeifanya Tanzania kuwa na uhusiano na pande zote mbili wakati wa Vita Baridi na hata sasa kama ilivyobainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mhe. Balozi Augustine Mahiga alipowasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2016/2017.

.....................................

Mwandishi wa makala hii ni mwanahistoria na mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kwa barua pepe: tanzaniahistory@yahoo.com
Tupe maoni yako.