Jumapili, 5 Juni 2016

Bondia MUHAMMAD ALI na Diplomasia ya TANZANIA

Tanzania imekuwa ikifuata sera ya kutofungamana na upande wowote tangu miaka ya 1960 mpaka sasa. Hali hiyo imeifanya Tanzania kuwa na uhusiano na pande zote mbili wakati wa Vita Baridi (Cold War).

Vita Baridi ni mvutano wa kisiasa na kijeshi baina ya Kambi ya Magharibi (Western Bloc) iliyoongozwa na Marekani na Kambi ya Mashariki (Eastern Bloc) iliyoongozwa na Urusi (USSR). Marekani na wenzake walifuata uchumi wa kibepari (capitalist economy) wakati Urusi na washirika wake wakifuata uchumi wa kijamaa (socialist economy). Mvutano huo ulianza mara baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia (WW II) hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Mwaka 1979 Urusi (USSR) iliivamia Afghanistan. Marekani ilipinga vikali kitendo hicho. Wakati huohuo Urusi ilikuwa inafanya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ambayo ilipangwa kufanyika jijini Moscow mwaka unaofuata 1980.

Ili kupata uungwaji mkono kukwamisha michezo hiyo ya olimpiki jijini Moscow mwaka 1980, Marekani ilianza kampeni zake kushawishi baadhi ya nchi zisishiriki mashindano hayo. Katika kujaribu kufanikisha hilo, rais wa Marekani wa wakati huo Jimmy Carter alimtuma bondia MUHAMMAD ALI kutembelea baadhi ya nchi ili aweze kuzishawishi zisusie mashindano hayo maarufu duniani.

Mnamo tarehe 2 Februari 1980 MUHAMMAD ALI aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (DIA) nchini Tanzania na kulakiwa na Chediel Mgonja, Waziri wa Utamaduni, Vijana na Michezo. MUHAMMAD ALI alipaswa kulakiwa angalau na Waziri wa Mambo ya Nje kwa kuwa ujio wake nchini Tanzania ulikuwa wa kidiplomasia na siyo michezo.

Lengo kuu la bondia huyo lilikuwa kuwasilisha ujumbe wa Rais wa Marekani Jimmy Carter kwa Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanzania wakati huo. ALI alitaka amshawishi Mwalimu Julius Nyerere ili Tanzania isishiriki Michezo ya Olimpiki iliyopangwa kufanyika jijini Moscow, Urusi mwaka huo. Pamoja na jitihada nyingi zilizofanywa na maafisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kumshawishi Mwalimu Julius Nyerere kuonana na mwanamasumbwi MUHAMMAD ALI, Mwalimu Nyerere alikataa kabisa ombi hilo.

Baada ya 'bondia mwanadiplomasia' MUHAMMAD ALI kushindwa kuonana na Mwalimu Julius Nyerere, aliamua kuondoka nchini Tanzania na kuelekea nchini Kenya ambapo alilakiwa na Rais Daniel Arap Moi. Kenya ilikubali ushawishi wa Marekani na kususia Michezo ya Olimpiki ya mwaka huo. Tanzania ilikataa ushawishi wa Marekani na kushiriki Michezo ya Olimpiki jijini Moscow, Urusi mwaka huo ambapo ilijinyakulia medali mbili za fedha kupitia wanariadha mashuhuri Suleiman Nyambui na Filbert Bayi.

Diplomasia huhitaji ushawishi. Marekani ilimtumia bondia MUHAMMAD ALI kutokana na umaarufu wake kipindi hicho na pengine kwa kuwa ni Mmarekani mweusi ili nchi za Afrika zishawishike kirahisi. Pia itakumbukwa mwaka 1974 Rais wa Zaire (sasa DRC) Mobutu Seseseko aliandaa mpambano mkali baina ya mabondia wa Marekani MUHAMMAD ALI na George Foreman. Mpambano huo maarufu uliotajwa kuwa "mpambano mkubwa wa karne ya 20" uliofanyika Kinshasa, Zaire na kupewa jina la 'THE RUMBLE IN THE JUNGLE.' ALI alishinda katika mpambano huo kumwongezea umaarufu mkubwa barani Afrika na duniani kote.

Tanzania haikuwa na maslahi yoyote katika uvamizi wa Urusi nchini Afghanistan. Pia Tanzania haikuona sababu yoyote kwanini ikubali ushawishi wa Marekani kususia Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1980. Haya yote yametokana na sera kigeni ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote. Tanzania imekuwa ikifuata sera hiyo tangu miaka ya 1960. Sera hiyo imeifanya Tanzania kuwa na uhusiano na pande zote mbili wakati wa Vita Baridi na hata sasa kama ilivyobainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mhe. Balozi Augustine Mahiga alipowasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2016/2017.

.....................................

Mwandishi wa makala hii ni mwanahistoria na mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kwa barua pepe: tanzaniahistory@yahoo.com
Tupe maoni yako.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni